Ofisi ya Rais – TAMISEMI ina mfumo wake wa mtandaoni wa kupokea maombi ya ajira za walimu (Elimu) na watumishi wa afya (Afya) zinazotangazwa kwa utaratibu wa kujitolea au mkataba. Mwongozo huu unaeleza jinsi ya kujisajili, kuingia na kukamilisha maombi kwenye mfumo huo.
Mfumo upi utumie?
- ajira.tamisemi.go.tz: "Mfumo wa Maombi ya Ajira ya Kujitolea/Mkataba" wa TAMISEMI, kwa nafasi za Elimu na Afya zinazotangazwa na TAMISEMI.
- portal.ajira.go.tz (Ajira Portal ya PSRS): kwa nafasi nyingi za ajira za kudumu serikalini. Soma mwongozo wa Ajira Portal.
Daima soma tangazo husika: linataja wazi mfumo wa kutumia na tarehe ya mwisho.
Hatua za kujisajili na kuomba (TAMISEMI)
- Fungua ajira.tamisemi.go.tz na uchague aina ya maombi: AFYA au ELIMU.
- Kama ni mwombaji mpya, bofya Jisajili (juu kulia) kuanza usajili.
- Ukishasajiliwa, ingia kwa kutumia namba ya NIDA au barua pepe uliyotumia kujisajili kama jina la mtumiaji (username), pamoja na nywila (password). Huijui namba yako ya NIDA? Soma jinsi ya kupata namba ya NIDA mtandaoni.
- Kamilisha taarifa zote zinazohitajika na uambatishe vyeti vinavyosomeka vizuri.
- Tuma maombi kabla ya tarehe ya mwisho. Kwa mujibu wa maelekezo ya mfumo, maombi yasiyokamilika hayafanyiwi kazi.
Maelekezo muhimu kutoka kwenye mfumo
- Soma na kuelewa vizuri tangazo kabla ya kutuma maombi.
- Hakikisha vyeti ulivyoambatanisha vinasomeka.
- Kuwasilisha taarifa za kughushi kunaweza kusababisha hatua za kisheria.
- Umesahau nywila? Tumia kiungo cha Badili Nywila kwenye ukurasa wa kuingia.
Msaada
Kwa mujibu wa mfumo wa TAMISEMI, huduma kwa mteja inapatikana kupitia simu 026 216 0210 au 0735 160 210.
Soma pia: Mfano wa barua ya maombi na CV | Maswali ya usaili | Ajira mpya serikalini
Comments
Comments
Post a Comment